Jumapili, 5 Aprili 2020

ATHARI ZA UHARIBIFU WA MISITU AMBAZO HAZIKO WAZI SANA


ATHARI ZA UHARIBIFU WA MISITU AMBAZO HAZIKO WAZI SANA
Misitu ni uhai kama inavojulikana na watu kwa asilimia kubwa na pia ikiwa ndio kauli mbiu ya wakala wa huduma za misitu Tanzania  TFS. Zamani uhitaji wa kupanda miti haukuwepo kutokana na kuwa misitu ilikuwa mingi na matumizi yalikuwa yako chini kutokana na idadi ya watu lakini pia maendeleo yanayohitaji bidhaa hizi za misitu kama malighafi za kuzalishia bidhaa hizo. Kwa kipindi tulichopo sasa kutokana na hali halisi kubalika tumeingia katika janga la kupoteza misitu kwa asilimia kubwa sana na hali hiyo kupelekea kuwa na mabadiliko ya tabia nchi hivyo kupelekea kuwa na mikakati ya kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabia nchi ikiwa ni pamoja na upandaji wa miti kwa kiasi kikubwa na kulida misitu ile ambayo bado imesalia kusudi isiweze kuvamiwa tena. Na ahgenda hii imekuwa ya kimataifa kwani na Afrika kuwa mhanga mkubwa wa mabadiliko ya tabia nchi lakini nchi nyingine zote duniani nazo zanpatwa na madhara hayo kwa namna moja au nyingine.  
Athari za mabadiliko ya tabia nchi ambayo husababishwa na uharibifu wa mazingira hasa uharibifu wa misitu ambazo wengi tunazifahamu ikiwa ni pamoja na kukosekana kwa mvua ambayo husababisha ukame mkubwa na kukausha mimea lakini pia kuharibu makazi ya viumbe hai kama ndege na vinginevyo. Joto kuongezeka na kusababisha mgonjwa ya Ngozi na madhara mengine ambayo hayakuwepo kabla, ongezeko la wadudu katika kilimo inayopelekea wakulima wa hali ya chini licha ya kuathiriwa na ukame ila hata kule kidogo ambacho wanakipata huharibiwa na wadudu na kufanya kuwa na uhitaji wa chakula kwa kiasi kikubwa.
Pamoja na athari zote hizo ila kumekuwa na athari moja ambayo ni kubwa ila watu wanashindwa kuitambua kwa urahisi kuwa nayo pia ni kutokana na uharibifu wa mazingira hasa katika eneo la uoto wa asili “Biodiversity” hili ni eneo muhimu sana katika kukamilisha kitu tunachoita msitu. Labda tukumbushane tofauti ya hizi aina mbili za misitu na kwann zikatengwa kuwa ni vitu viwili tofauti. Misitu ya asili na misitu ya kupandwa, misitu ya asili maana yake ni miti iliyofungana lakini pia chini kuna uoto unaofunika ardhi “trees with vegetation cover” na msitu wa kupandwa ni miti iliyopandwa kwa nafasi na kupaliliwa na hivyo kukosekana ule uoto unaofunika ardhi.
Aina zote mbili za misitu zinafaida ya kuleta mvua, kukabiliana na tatizo la ongezeko la joto, kunyonya hewa chafu inayotoka viwandani na kupendezesha mazingira yetu. Faida ambayo misitu ya asili inaizidi misitu ya kupandwa ni ile ya uwepo wa uoto wa asili unaofunika ardhi. Hii faida yake huonekana pale mvua inaponyesha utaona katika msitu wa kupandwa maji yanayotiririka ni mengi kuliko maji yanayotiririka katika msitu wa asili. Tofauti hii husababishwa na katika msitu wa asili tone linapodondoka linalazimishwa kuzama chini kwani halipati nafasi ya kuungana na matone mengine kutengeneza maji mengi na kuanza kutembea ila katika misitu ya kupandwa tone linapodondoka linaruka na kupata nafasi ya kukutana na tone jingine na hivyo kutengeneza maji na kuanza kutembembea kuelekea mteremko ulipo na mwisho wa siku hutengeneza mfereji na mwisho korongo na kuleta mafuriko huko mabondeni.
Hata hivyo kinachosikitisha sana kwa sasa hata hii misitu ya asili asilimia kubwa imekuwa kama misitu ya kupandwa na kuwa na tabia za misitu ya kupandwa japo inaundwa na misitu ya asili. Hii yote imetokana na shughuli za kibinadamu zinazofanyka katika misitu hiyo ikiwa kubwa Zaidi ni ufugaji na uchungaji wa mifugo unaoharibu kwa kiasi kikubwa uoto huo wa asili unaofunika ardhi. Hivyo unaweza pita kwa mbali ukaona miti imefunga vizuri ukajua hapo kuna msitu mzuri wa asili lakini ukisogea karibu unakutana na ardhi ikiwa uchi na kuondoa maana yote ya msitu wa asili na kuwa kama msitu wa kapandwa tu.
Kwa mujibu wa wazee wa zamani ambao bado wapo wanasema kuwa hawajashtushwa na mvua hizi kubwa zinazoendelea kunyesha kwa sasa ila kinachowashangaza ni mafuliko yanayotokea kwani hawajawahi kuyashuhudia kabla maana mashamba yanajaa maji n ahata kilimo kimekuwa changamoto kubwa kwao. Wanasema hata mwaka 1998 iliponyesha mvua kubwa ya elninyo maji hayakuwa mengi kiasi hiki ila kwa hii ya mwaka huu imekuwa ya kushangaza kidogo kwao. Hapa ndo unagundua sasa kuwa uharibifu wa uoto wa asili umechangia kiasi kikubwa katika kusababisha maji kutiririka kwa kasi kutoka milimani na kusambabisha mafuriko, uharibifu wa miundo mbinu na majanga mengine mengi.
Ufugaji ni mzuri na una tija kwa wananchi wenyewe na pia kwa taifa kwa ujumla kama ukifanywa kwa kuzingatia usalama wa mazingira yetu hususani katika misitu yetu ya asili. Lakini kama tusipolifanyia kazi hili mapema tutegemee kila mvua zitakapokuwa zinanyesha basi kutakuwa na madhara kadha wa kadha kwa wananchi na hata kwa serikali kwa ajili ya kutengeneza miundo mbinu inayoharibiwa na mvua kila wakati.
Rai yangu kwa mamlaka zinazohusika tunajitahidi kuhamasisha watu kupanda miti ili kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi tusisahau kuilinda misitu ya asili na uoto wake kwa vyote vina umuhimu mkubwa sana kwa maendeleo ya taifa na wananchi wake kwa ujumla. Hivyo kila mtu apande miti mingi kadri anavoweza lakini pia tuwajibike wote katika kuitunza misitu ya asili iliyopo kusudi kuepukana na haya yote yanayotokea sasa hivi.
Mungu ibariki Tanzania,
Mungu ibariki Afrika.
Imeandika na Martin Njau,
0717599375/0753989840 njaumartin48@gmail.com
Mwanaharakati wa mazingira na bwana Misitu.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni