“TELL THEM TO PROTECT ME AND I WILL PROTECT THEM TOO”
“WAAMBIE WANILINDE NAMI NITAWALINDA
PIA”
Kulinda, kulindwa, kulindiwa, ulindaji, etc yote haya yanatokana na mzizi wa neno “LINDA”. Linda” ila sio jina la mtu” kwa maana rahisi ni kitendo cha kuwekea ulinzi kitu fulani ili kisipatwe na matatizo au kisisumbuliwe na vitu vingine. Unapotaka kulinda kitu ni lazima ukifahamu kitu chenyewe kwa undani ilkiwa ni pamoja na umuhimu wake kwako ikimaanisha faida zake. Lakini kikubwa ni kuwa unapohitaji kulinda kitu flani lazima ujue njia zipi zinazotumika kukilinda kitu hicho kikamilifu. Hii itakusaidia kupata mtiririko mzuri wa kukilinda kitu hicho ili kuweza kukupatia faida zaidi na zaidi.
Mazingira ni kitu cha muhimu sana katika maisha ya binadamu na ikiwa yanawekwa katika hali ambayo sio salama basi husababisha usalama kupotea pia kwa wale wanaoyatumia. Lakini pia katika mazingira ndio tunapopata vitu vingine vingi ikiwepo pia misitu na mengine mengi ambayo tunayapata pale tunapoweka mazingira sawa.
Lakini hapa ninachotaka kukizungumzia zaidi ni utunzaji wa mazingira kwa ujumla lakini nikiegamia sana katika utunzaji wa misitu yetu. Nadhani wote tunafahamu umuhimu wa kutunza misitu na kila siku tunakumbushana kuhusu kitu hicho ambacho ni faida kwa wote. Ipo sauti inayoita kutoka katika mazingira au katika misitu ikisema kuwa “WAAMBIE WAKINILINDA NAMI NITAWALINDA PIA” hii ndo inayonisukuma kuandika hiki kwenu leo wote wana mazingira kwa ujumla wetu.
Nakumbuka nishawahi kuandika kuhusu kila mtu ni mwanamazingira kwa asili ila kuwa bwana/bibi misitu ni chaguo la mtu kusomea kitu hicho. Hii ilikuwa na maana kwamba kila mtu anaishi katika mazingira ila wanaishi misituni ni wachache sana na wengi ni wanyama. Hivyo tunapaswa kuwa na elimu ya utunzaji wa mazingira hata bila ya kuipata kutoka darasani kwani ni faida ya kila mmoja wetu katika maisha yake.
Hivi karibuni tumekuwa tukisikia kuhusu mabadiliko ya tabia nchi yanayoendelea kutokea kila mara na kuzidi kwa kasi. Haya yote yanasababishwa na uharibifu wa mazingira unaofanyika katika maeneo mbalimbali ya dunia. Tumekuwa tushuhudia ongezeko la joto ambalo inakadiriwa kuwa limeongezeka kwa takribani nyuzi 3 hadi 5 na kusababisa kuyeyuka kwa barafu ambazo zipo kwenye milima mirefu kama vile mlima Evarist uliopo bara la Asia na pia mlima Kilimanjaro ambao upo katika nchi yetu.
Ila sio hilo tu bali tumekuwa tukishuhudia barafu ya bahari ya atlantiki inavyozidi kupungua na kusababisha kina cha maji kuendelea kupanda na kufunika baadhi ya visiwa ambavyo vilikuwa vinaonekana hapo mwanzo. Hiyo yote ni sababu ya ongezeko la joto ambalo linasababishwa na uharibifu wa mazingira hasa uharibifu wa misitu. Na huu husababishwa na shughuli mbalimbali za kijamii zinazofanyika katika maeneo ya makazi na hata shughuli za kibiashara kama vile viwanda na pia usafirishaji.
Lakini hali hii mbaya ya tishio kwa taifa na hata kwa dunia nzima ni lazima kuwepo na juhudi za makusudi za kuweza kuipunguza kama si kuitokomeza kabisa. Inawezekana endapo kila mtu atachukua hatua madhubuti juu ya hili ili kupunguza athari hizi zinazoikabili dunia kwa ujumla. Kinachotakiwa kila mtu amfikirie mwenzake kwamba anaumia kiasi gani juu ya uharibifu huu na aifanye hali ile iwe kama yake kwani nchi nyingi zilizoendelea ndio zinaongoza kwa uchafuzi wa mazingira ila madhara mengi huja kwa wale wasio na hatia.
Hivyo basi sote na tuisikie sauti hii inayoita kutoka katika mazingira yetu na hata katika misitu yetu kuwa tukiitunza na kuilinda basi nayo itatutunza na kutulinda na kutuweka katika hali nzuri isiyo ya hatari na mashaka kama tulivyo sasa. Kwani mvua zitakuwa za kutosha na kwa wakati, maji hayatakuwa na tabu katika upatikanaji wake, joto litapungua ila pia ile barafu iliyokuwa inayeyuka kutoka katika milima mirefu itaacha kuyeyuka tena.
Tuyapende mazingira, tuipende misitu, tuwe marafiki wao kwani tukiwa maadui wao nao watakuwa maadui wetu. Wito wangu kwa kila mmoja ona uchungu kwa kizazi hiki na kile kijacho wasije kuta simulizi tu kwa yote yaliyotokea. Ni wakati wangu na wako kusitisha athari hizi za mabadiliko ya tabia nchi kuendelea kutuumiza. Anza sasa bado hujachelewa tunza mazingira, tunza misitu, panda miti kwa wingi epuka athari za mabadiliko ya tabia nchi.
Kila mtu na asikie sauti hii inayotoka katika mazingira na misitu ya kuwa “mkitulinda nasi tutawalinda” tukiisikia na kuifanyia kazi basi tutaona mabadiliko.
Kumbuka ustawi wa mazingira na misitu uko juu yangu na yako tuchukue hatua.
Mungu ibariki Afrika
Mungu ibariki Tanzania.
Njau
Martin
+255
717 599 375

Hakuna maoni:
Chapisha Maoni