“MDA MWINGINE
NI BORA KUOKOTA NA KUBEBA MOJA YENYE FAIDA NA MANUFAA KWAKO KULIKO KUKUMBATIA
KUMI INAYOKUUMIZA NA KUKURUDISHA NYUMA”
Kama ilivyo ada
ya safu yetu ya kujuzana moja na mbili ili hali ni katika kubadilishana mawazo
na kuongezeana uelewa katika baadhi ya mambo ya kimaisha. Kwanza nianze kwa
kumshukuru Mungu kwa kutujalia afya mjema na nguvu nyingi kwa ajili ya utukufu
wake. Lakini pia kwa ajili ya kutufanya tuendelee kutimiza wajibu wetu kama
wanadamu. Ni matumaini yangu kuwa u mzima wa afya na unaendelea vizuri na
majukumu yako, kama huko poa basi Mungu akujalie upate nafuu mapema. Karibu
tena katika safu yetu ya kujuzana.
Mada ya leo
inahusu kuachia vitu ambavyo kwa wakati mwingine huwa havina faida kwetu. Mada
inasomeka hivi “mda mwingine ni bora kuokota na kubeba moja yenye manufaa na
faida kwako kuliko kukumbatia kumi inayokuumiza na kukurudisha nyuma”. Mara
nyingi tumekuwa tukishikilia vitu ambavyo huwa havina manufaa kwetu ila
kutokana na kuwa na matumaini potofu au matumaini yaliyokufa ambayo hayana
macho tunajikuta tukiendelea kuyakumbatia tena kwa mikono miwili. Hii ni
kawaida kwa kila mtu na hutokana na labda mtu huyo alikuwa na matarajio flani
juu ya kitu hicho lakini kiukweli ni kwamba uwezekano wa kupata au kufanikiwa
kufikia matarajio yake ni hafifu sana. Lakini kutokana na woga wa kwamba
inawezekana ni nyundo ya mwisho jiwe litapasuka lakini unajikuta bado sana na
kuzidi kupoteza muda juu ya hilo.
Kiukweli watu
wengi wanakuwa na maumivu hasa ya ndani kwa ajili ya hilo kwani watu
wanahifadhi vitu ambavyo kiukweli havina faida yoyote na kuna uwezekano wa
kwamba vitu hivyo vinaendelea kumuumiza mtu na anashindwa kuviacha kutokana na
kile kinachozaniwa kuwa labda mafanikio yapo karibu na unajipa moyo wa
kuendelea kusubiri tena. Sisemi kuwa ni kosa kufanya hivyo ila kuna kila sababu
ya kubadilika na kuanza upya kwani kufanya hivyo ni sawa na kusubiria mbegu
iliyooza iweze kuota kitu ambacho ni upotezaji wa mda. Kinachotakiwa ni
kuifukua na kupanda nyingine kana kwamba hiyo haitoshi basi pia ni lazima
uangalie ni kitu gani ambacho kimesababisha kuweza kuoza kwa mbegu hiyo.
Ukimuuliza mtoto
kati ya moja na kumi kubwa ni ipi lazima atakujibu kuwa ni kumi ndo kubwa.
Lakini unapomuuliza mtu mzima kati ya moja na kumi ipi kubwa kama anafikiria
vizuri basi atakuuliza katika upande gani? Maana kuna wakati kumi inakuwa kubwa
na wakati mwingine moja inakuwa kubwa zaidi ya kumi kutokana na eneo ambalo
imetumika. Hii ina maana kuwa kuna wakati inabidi kuachia kumi ambayo inakuwa
haina faida kwa wakati huo na kuokota moja ambayo ina faida na maendeleo bora
kwako.
Marafiki ni
vizuri kuwa nao ila unapoona kuwa upo na marafiki ambao sio sahihi ni bora
kuwaachia na kutengeneza nafasi kwa ajili ya marafiki ambao wanafaida kwako na
wanakusaidia kufikia malengo yako na kukushauri pale unapokosea. Pia kama
rafiki lazima awe anajali na kuona ya kuwa ana kila sababu ya kukufanya
ujisikie kuwa rafiki yake kwani unaweza kuwa na rafiki lakini usiweze kuhisi
uwepo wa huyo rafiki yako kwani mchango wake unakuwa mdogo sana kwako.kuwa
rafiki sio jina tu kuwa flani ni rafiki yangu ila je kuna vitu vyovyote ambavyo
vinaonesha uhalisia wa urafiki wenu? Urafiki ni zaidi ya jina. Kubeba watu
ambao hawana faida maishani mwako ni uzembe na uvivu wa kutafuta marafiki wenye
tija katika maisha yako. Ni sawa na kuogopa kwenda shamba eti kisa mvua
inanyesha.
Tengeneza nafasi
kwa ajili ya marafiki walio na tija katika maisha yako achana na kukumbatia
marafiki ambao hawana maana katika maisha yako kwani wanaweza kuwa
wanakuchelewesha kule unakoenda na mwisho wa siku kumbe hawaendi huko. Na baada
ya hapo ni kukucheka kuwa muone alivyoaibika alikuwa anajifanya anaweza sana
kumbe hamna kitu. Kaa mbali nao sana kwani sio watu wazuri hata kidogo kwa
maendeleo ya afya yako ya kimaendeleo. Fanya mabadiliko sasa ya kuacha
kukumbatia vitu ambavyo havina faida
kwetu na vinatupotezea muda. Sasa ni muda sahihi wa kukaribisha vitu ambavyo
vina faida kwetu hata kama vinaonekana kuwa vidogo ila vina faida kuliko
kukumbatia hivyo vikubwa lakini havina faida.
Njau M
0717599375
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni